Zaburi 98
ONMM1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; kitanga chake cha kuume na mkono wake mtakatifu umemfanyia wokovu. 2 Mwenyezi Mungu ameufanya wokovu wake ujulikane na amedhihirisha haki yake kwa mataifa. 3 Ameukumbuka upendo wake na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli; miisho yote ya dunia imeuona wokovu wa Mungu wetu. 4 Mpigieni Mwenyezi Mungu kelele za shangwe, dunia yote, ipaze sauti kwa nyimbo za shangwe na vinanda; 5 mwimbieni Mwenyezi Mungu kwa kinubi, kwa kinubi na sauti za kuimba, 6 kwa tarumbeta na mvumo wa baragumu za pembe za kondoo dume: shangilieni kwa furaha mbele za Mwenyezi Mungu, aliye Mfalme. 7 Bahari na ivume na kila kilicho ndani yake, dunia na wote wanaoishi ndani yake. 8 Mito na ipige makofi, milima na iimbe pamoja kwa furaha, 9 vyote na viimbe mbele za Mwenyezi Mungu, kwa maana yuaja kuhukumu dunia. Atahukumu dunia kwa haki na mataifa kwa haki.
