Zaburi 96
ONMM1 Mwimbieni Mwenyezi Mungu wimbo mpya; mwimbieni Mwenyezi Mungu dunia yote. 2 Mwimbieni Mwenyezi Mungu, lisifuni jina lake; tangazeni wokovu wake siku baada ya siku. 3 Tangazeni utukufu wake katika mataifa, matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote. 4 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote; yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote. 5 Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu, lakini Mwenyezi Mungu aliziumba mbingu. 6 Fahari na enzi viko mbele yake; nguvu na utukufu vimo patakatifu pake. 7 Mpeni Mwenyezi Mungu, enyi jamaa za mataifa, mpeni Mwenyezi Mungu utukufu na nguvu. 8 Mpeni Mwenyezi Mungu utukufu unaostahili jina lake; leteni sadaka na mje katika nyua zake. 9 Mwabuduni Mwenyezi Mungu katika uzuri wa utakatifu wake; dunia yote na itetemeke mbele zake. 10 Semeni katika mataifa kwamba, “Mwenyezi Mungu anatawala.” Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa; atawahukumu watu kwa uadilifu. 11 Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi; bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake; 12 mashamba na yashangilie, pamoja na vyote vilivyomo. Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha; 13 itaimba mbele za Mwenyezi Mungu kwa maana anakuja, anakuja kuihukumu dunia. Ataihukumu dunia kwa haki, na mataifa katika kweli yake.
