Zaburi 86
ONMM1 Ee Mwenyezi Mungu, sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji. 2 Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, wewe ni Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako anayekutumaini. 3 Ee Bwana, nihurumie mimi, kwa maana ninakuita mchana kutwa. 4 Mpe mtumishi wako furaha, kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana, ninainua nafsi yangu. 5 Ee Bwana, wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao. 6 Ee Mwenyezi Mungu, sikia maombi yangu, sikiliza kilio changu unihurumie. 7 Katika siku ya shida yangu nitakuita, kwa maana wewe utanijibu. 8 Ee Bwana, katikati ya miungu hakuna kama wewe, hakuna matendo ya kulinganishwa na yako. 9 Ee Bwana, mataifa yote uliyoyafanya yatakuja na kuabudu mbele zako; wataliletea utukufu jina lako. 10 Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu. 11 Ee Mwenyezi Mungu, nifundishe njia yako, nami nitaenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako. 12 Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele. 13 Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka vilindi vya kaburi . 14 Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe. 15 Lakini wewe, Ee Bwana, ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu. 16 Nigeukie na unihurumie; mpe mtumishi wako nguvu zako, mwokoe mwana wa mjakazi wako . 17 Nipe ishara ya wema wako, ili adui zangu waione nao waaibishwe, kwa kuwa wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umenisaidia na kunifariji.
