Zaburi 53
ONMM1 Mpumbavu anasema moyoni mwake, “Hakuna Mungu.” Wameharibika, na njia zao ni za uovu kabisa, hakuna hata mmoja atendaye mema. 2 Mungu anawachungulia wanadamu chini kutoka mbinguni aone kama wako wenye akili, wowote wanaomtafuta Mungu. 3 Kila mmoja amegeukia mbali, wameharibika wote pamoja, hakuna atendaye mema. Naam, hakuna hata mmoja! 4 Je, watendao maovu kamwe hawatajifunza: wale ambao huwala watu wangu kama watu walavyo mkate, hao ambao hawamwiti Mungu? 5 Hapo waliingiwa na hofu kuu, ambapo hapakuwa na hofu. Mungu alitawanya mifupa ya wale waliokushambulia; uliwaaibisha, kwa sababu Mungu aliwadharau. 6 Laiti wokovu wa Israeli ungekuja kutoka Sayuni! Mungu anaporejesha wafungwa wa watu wake, Yakobo na ashangilie, Israeli na afurahi!
