Menu

Zaburi 138

ONMM

1 Nitakusifu wewe, Ee Mwenyezi Mungu, kwa moyo wangu wote, mbele ya “miungu” nitaimba sifa zako. 2 Nitasujudu nikielekea Hekalu lako takatifu, nami nitalisifu jina lako kwa ajili ya upendo wako na uaminifu, kwa maana umeitukuza ahadi yako zaidi ya jina lako. 3 Nilipoita, ulinijibu; ulinifanya jasiri na mwenye moyo hodari. 4 Wafalme wote wa dunia wakusifu wewe Ee Mwenyezi Mungu, wakati wanaposikia maneno ya kinywa chako. 5 Wao na waimbe kuhusu njia za Mwenyezi Mungu, kwa maana utukufu wa Mwenyezi Mungu ni mkuu. 6 Ingawa Mwenyezi Mungu yuko juu, humwangalia mnyonge, bali mwenye kiburi yeye anamjua kutokea mbali. 7 Nijapopita katikati ya shida, wewe unayahifadhi maisha yangu, unanyoosha mkono wako dhidi ya hasira ya adui zangu, kwa mkono wako wa kuume unaniokoa. 8 Mwenyezi Mungu atatimiza kusudi lake kwangu, Ee Mwenyezi Mungu, upendo wako wadumu milele: usiziache kazi za mikono yako.

Everything we make is available for free because of a generous community of supporters.

Donate