Zaburi 11
ONMM1 Kwa Mwenyezi Mungu ninakimbilia. Unawezaje basi kuniambia: “Ruka kama ndege utorokee kwenye mlima wako. 2 Hebu tazama, waovu wanapinda nyuta zao; wanaweka mishale kwenye nyuzi zake ili wakiwa gizani, wawapige walio wanyofu wa moyo. 3 Wakati misingi imeharibiwa, mwenye haki anaweza kufanya nini?" 4 Mwenyezi Mungu yuko ndani ya Hekalu lake takatifu; Mwenyezi Mungu yuko kwenye kiti chake cha enzi mbinguni. Huwaangalia wana wa watu, macho yake yanawachunguza. 5 Mwenyezi Mungu huwachunguza wenye haki, lakini nafsi yake inachukia waovu na wale wanaopenda mapigano. 6 Atawanyeshea waovu makaa ya moto mkali na kiberiti kinachowaka; upepo wenye joto kali ndio fungu lao. 7 Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye haki, yeye hupenda haki. Wanyofu watauona uso wake.
