Menu

Isaya 35

ONMM

1 Jangwa na nchi kame vitafurahi; nyika itashangilia na kuchanua maua. Kama waridi, 2 litachanua maua, litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha. Litapewa utukufu wa Lebanoni, fahari ya Karmeli na Sharoni; wataona utukufu wa Mwenyezi Mungu, fahari ya Mungu wetu. 3 Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea, 4 waambieni wale wenye mioyo ya hofu, “Kuweni hodari, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja kulipa kisasi, pamoja na ujira wake, atakuja na kuwaokoa." 5 Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa na masikio ya viziwi yatazibuliwa. 6 Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu, nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe. Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika, na vijito katika jangwa. 7 Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji, ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi. Maskani ya mbweha walikolala hapo awali patamea nyasi, matete na mafunjo. 8 Nako kutakuwa na njia kuu, nayo itaitwa Njia ya Utakatifu. Wasio safi hawatapita juu yake; itakuwa ya wale wanaotembea katika Njia Ile; yeye asafiriye juu yake, ajapokuwa mjinga, hatapotea. 9 Huko hakutakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapita njia hiyo; hawatapatikana humo. Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko, 10 waliokombolewa na Mwenyezi Mungu watarudi. Wataingia Sayuni wakiimba; furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao. Watapata furaha na shangwe; huzuni na majonzi vitakimbia.

Everything we make is available for free because of a generous community of supporters.

Donate